Jumatano 16 Aprili 2025 - 09:51
Muqawama wa kiislamu ni siri ya ushindi dhidi ya ukoloni na dhulma

Sheikh Ghazi Hanina, akieleza nafasi ya kihistoria na kidini ya Muqawama wa Kiislamu, alisisitiza kuwa: Nguvu yote ya Waislamu katika historia, hasa katika kukabiliana na wakoloni na dhulma, daima imejengwa juu ya misingi ya uadilifu na utetezi kwa wanyonge.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ghazi Hanina, Raisi wa Bodi ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, siku ya Jumatatu, katika kikao cha mtandaoni cha "Mkutano wa awali wa Hawza wa maonyesho wa Kimataifa ya Theolojia ya Mapambano" kilichokuwa na maudhui isemayo “Vipengele vya Kimapinduzi vya Theolojia ya Mapambano katika Historia,” alieleza nafasi ya kihistoria na kidini ya muqawama wa Kiislamu.

Akiashiria asili ya kujihami kwa mapambano yote ambayo Waislamu wameshiriki ndani yake katika historia kwa anuani ya uislamu halisi, alisisitiza kuwa: Uislamu haujawahi kuanzisha dhulma na uvamizi, na hautakuwa kamwe. Kwa mujibu wa maelezo yake, vita vyote vilivyopiganwa na waislamu vilikuwa ni kwa lengo la kuwatetea wanyonge na wadhulumiwa na kukabiliana na dhulma na uasi.

Raisi wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, kwa kunukuu Hadithi ya Qudsi inayosema: “Enyi waja wangu! Hakika Mimi nimejiharimishia dhulma na nimeiharamisha miongoni mwenu pia; basi msidhulumu,” alibainisha kuwa: Vita vya Kiislamu vimejengwa juu ya msingi wa uadilifu na utetezi halali, na kwa sababu hiyo vimekuwa vikihusiana na ushindi.

Sheikh Hanina aliendelea kuzungumzia uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa harakati ya muqawama na akasisitiza: Msaada huu ulianza tangu wakati wa Imam Khomeini (r.a) na umeendelea chini ya uongozi wa hekima wa Imam Khamenei.

Aliongeza kuwa: Kwa baraka za uungaji mkono huu, leo hii harakati ya muqawama imefikia hatua ya kumiliki silaha za hali ya juu kabisa na ina uwezo wa kulenga maeneo ya ndani kabisa ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Aidha, akitaja mfano wa ushindi wa kisasa, alirejelea mapambano ya “Kimbunga cha Al-Aqsa” na akaongeza kuwa: Operesheni hii imeendelea kwa zaidi ya miezi kumi na minane na imeusababishia hofu na mgawanyiko mkubwa wa ndani utawala wa Kizayuni.

Sheikh Hanina, akisisitiza kuwa mapambano hayatarudi nyuma kutoka katika misimamo yake, alisema kuwa: Njia ya Jihadi bado ipo wazi, na ahadi ya hakika ya Mwenyezi Mungu kuhusu ushindi iko karibu; kama ambavyo Qur’ani Tukufu inasema: “Kama mnamnusuru Mwenyezi Mungu, Atakusaidieni na Ataziimarisha nyayo zenu.”

Akiashiria lengo la pamoja la dini zote za mbinguni na Mitume wa Mwenyezi Mungu, alisisitiza kuwa: Wote hao wametumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya heshima, utukufu, na kuinuliwa kwa hadhi ya mwanadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha